Huenda idadi ya Watanzania wanaotumia umeme ya gridi ya Taifa ikaongezeka siku za hivi karibuni baada ya Benki ya Dunia kutoa ufadhili kwa ajili kupeleka umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa.
Bodi ya benki hiyo juzi Septemba 26, 2022 imeidhinisha imeongeza ufadhili wa Dola za Marekani milioni 335 (Sh770.5 bilioni) kwa ajili ya kupanua gridi ya Taifa ili kuwezesha upatikanaji wa umeme na usambazaji wa nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini.
Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA) iliyo chini ya benki hiyo inashirikiana na Mpango wa Kuendeleza na Kusambaza Umeme Tanzania (TREEP) ili kuunganisha msongo wa umeme wa kilomita milioni 1.6.
Umeme huo utazifikia shule 8,500 na vituo vya afya 2,500 pamoja na kuwezesha upatikanaji wa nishati mbadala za kupikia zitakazosaidia kaya za vijijini.
Pamoja na maendeleo makubwa ya Tanzania katika kuongeza upatikanaji wa umeme kutoka asilimia 7 mwaka 2011 hadi asilimia 38 mwaka 2020, bado kuna pengo kubwa lililopo kati ya viwango vya upatikanaji wa umeme mijini na vijijini.
“Kuongeza upatikanaji wa nishati ya kisasa ni sehemu muhimu ya mpango wa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu wa Serikali ya Tanzania,” amesema Preeti Arora, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania.
Fedha hizo zilizotolewa na zimeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 209 zilizotolewa Mei, 2016 ambazo ziliwezesha programu ya TREEP kuanza kutekelezwa.
Walio nje ya gridi ya Taifa kufikiwa
Ufadhili huo wenye lengo la kupanua gridi ya Taifa utawafikia wananchi ambao awali hawakufikiwa na gridi hiyo hali iliyosababisha kaya hizo kubaki bila nishati ya umeme.
Jenny Hasselsten, Mchumi Mwandamizi wa Nishati wa Benki ya Dunia na Kiongozi wa Timu ya TREEP, amesema asilimia 15 zaidi ya watu ambao hawakufikiwa na gridi ya Taifa wanufaika na upanuzi wa gridi hiyo na kufanya idadi ya watakaofikiwa kuongezeka.
“Kwa ufadhili huu wa ziada, TREEP inatarajiwa kusambaza umeme kwa asilimia 15 ya watu waliopo nje ya gridi ya Taifa ambayo itaongeza kiwango cha ufikiaji nchini Tanzania kutoka asilimia 38 hadi asilimia 45,” anasema Jenny.
IDA iliyo chini ya Benki ya Dunia ilianzishwa mwaka wa 1960, ili kusaidia nchi maskini zaidi duniani kwa kutoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ili kuwezesha miradi na programu zinazokuza ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, na kuboresha maisha ya watu maskini.