Benki ya Dunia imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 200 (Sh bilioni 466.387) kugharamia mradi wa Bonde la Msimbazi ili kuepuka mafuriko na kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kukabili ongezeko la watu.
Fedha hizo zimeidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa benki hiyo Septemba 30, mwaka huu. Gharama za mradi wote ni Dola za Marekani milioni 260 sawa na sh bilioni 606.429.
Dola milioni 60 zitatolewa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa la Hispania ambalo litatoa Dola milioni 30 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi itatoa ruzuku ya Euro milioni 30.
Benki ya Dunia imeeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kunusuru watu zaidi ya 30,000 wanaokabiliwa na changamoto ya mafuriko ya Mto Msimbazi zikiwamo jamii nyingi za kipato cha chini.
Kupitia fedha hizo, eneo ambalo hukumbwa na mafuriko katikati ya jiji litabadilishwa kuwa la kijani, la biashara na makazi ambalo litabufaisha wakazi wa Dar es Salaam.