Dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha umeme unafika mpaka vijijini kwa namna yoyote inaenda kutimia, baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusaini mkataba na Umoja wa Ulaya (EU) wa Sh. bilioni 34 kwa ajili ya mradi wa kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji, ili kupunguza maambukizi ya magonjwa ya milipuko ikiwamo UVIKO-19.
Mradi huo utanufaisha hospitali sita, vituo vya afya 57 na miradi ya maji 363 ambayo itaunganishwa kupata huduma ya nishati ya umeme katika mikoa 25 nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassab Saidy, alisema kazi hiyo itafanywa na makandarasi wazawa watatu kusambaza umeme katika vituo vya afya na vituo vya maji.
Alisema mradi huo ni mpango maalumu ambao ulilenga kusaidia jitihada za serikali kuzuia magonjwa ya maambukizi ikiwamo Uviko-19 na mengine.