Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ushauri kwa viongozi wa wanawake Afrika akitaja sifa ni kuwa msikivu, mwelevu, muwazi na mtu ambaye yupo tayari kujifunza.
Akizungumza kwenye Kongamano la Nne La Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Afrika leo tarehe 03 Desemba, 2022 Zanzibar, Rais Samia alijibu swali hilo kwa kutaja miongozo takribani 6 ya kuwa kiongozi bora.
“Kwa uzoefu wangu kwanza kabisa ni kujitambua mwenyewe na lengo lako, kwakufahamu hilo lazima uwe mnyeyekevu uweze kuwasikiliza watu zaidi na kuzungumza kidogo kuwasikiliza hata wale ambao unadhani ni wapumbavu kwa sababu wanaweza kuwa na kitu cha msingi cha kujifunza kutoka kwao,
“La pili kuelewa jamii yako ambayo unataka kuwasiliana nao sio kwa namna yoyote kwa sababu hapa Afrika tuna tamaduni zetu, mila zetu lazima tujue namna ambavyo tunaweza kuzungumza na watu tulionao,
“La tatu, kujifunza kutoka kwa watangulizi, wale ambao wanafahamu taasisi unayoifanyia kazi wapo wazoefu watangulizi ambao wamekuwa kwenye taasisi kwa muda mrefu wasikilize lakini usifanye wakulazimishe ufuate matakwa yao lakini tafuta njia yako,
“Uwe wazi katika utendaji wako, uwe wazi kabisa kuhusu mfumo wa utendaji wako kwamba unalitaka hili na hutaki hiki, sitaki kutajwa hivi nataka nitajwe vile uwe wazi kuhusu namna mfumo wa uongozi,
“Usilazimishe watu usiwe na udikteta, shirikisha kuwa na mbinu shirikishi usiagize kafanye hili kafanye lile waulize tukifanye hili itakuwaje alafu waachie watekeleze lakini kama ukiwa na udikteta safari yako itakuwa ni fupi.'” alisema Rais Samia.
Aidha, aliwataka viongozi wanawake barani Afrika kuhakikisha wanainuana ili kupaza sauti za wanawake wote na sio kudidimizana.
“Unapokutana na wanawake wenzako saidia kuwainua, wainuie usiwasukumizie chini kwa sababu ukiwainua mtakua wengi mkiwa juu kwahiyo idadi yenu itakuwa kubwa na mtakuwa na sauti kubwa lakini ukiwasukuma wanawake wenzako chini hutokuwa na sauti kubwa,” alisisitiza