Fahamu jinsi ya kuepuka maumivu ya Januari 2023

HomeKitaifa

Fahamu jinsi ya kuepuka maumivu ya Januari 2023

‘Njaanuari’ ndivyo ambavyo baadhi ya watu huuita Januari ambao kwa mujibu wa kalenda ndiyo mwezi wa kwanza wa mwaka.

Jina hilo linaashiria machungu ya matumizi ya pesa ambayo kwa watu wengi huonekana makubwa kuliko vipato vyao.

Baadhi ya matumizi ya fedha yaliyopo Januari ni pamoja na karo za shule, kodi ya pango, gharama ya shughuli za kilimo, pamoja na gharama ya safari, ambayo hutumia kiasi kikubwa cha fedha na kuufanya mwezi huo kuonekana mrefu au mgumu.

Pamoja na kuwepo na matumizi mengi yanayohitaji fedha mwezi huo, upo uwezekano wa kupunguza machungu kwa kufanya mambo kadhaa yanayashauriwa na wataalamu wa masuala ya uchumi.

Kupanga bajeti mapema

Ni wazi kuwa matumizi mengi ya Januari huwa yanafahamika mapema, hivyo ni muhimu kuandaa bajeti ya matumizi husika ili kuepusha mkanganyiko wa matumizi.

Tovuti ya Fikra za kitajiri ambayo huchapisha makala za ushauri wa namna ya kukua kiuchumi inaeleza kuwa njia rahisi zaidi ni kujiwekea bajeti ya mwaka mzima.

“Mahitaji ya ada za wanafunzi au malipo ya kodi yanatakiwa kuanza kuandaliwa kabla ya mwisho wa mwaka ili itakapofika muda wake liwe ni suala la kukamilisha malipo,” inaandika tovuti hiyo.

Punguza matumizi ya mwisho wa mwaka

Ili kuuanza mwezi Januari vema ni muhimu kupunguza matumizi ambayo yatatumia kiasi kikubwa cha fedha mwishoni mwa Disemba ambao huisha kwa sherehe kama Krismas pamoja na mwaka mpya.

Watu wengi huingia gharama katika kununua vyakula na vinywaji, mavazi, au zawadi kwa ajili ya watu wawapendao bila kusahau nauli za safari kwenda kusheherekea sehemu mbalimbali.

Kwa kuzingatia hali ya kipato chako pamoja na bajeti uliyojiwekea, unaweza kuepuka matumizi yasiyo ya lazima, au  kufanya manunuzi ya jumla ambapo vitu huuzwa kwa bei nafuu zaidi jambo litakalosaidia kuokoa kiasi fulani cha fedha.

Fanya manunuzi mapema

Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji mwishoni mwa mwaka, baadhi ya wafanya biashara hutumia fursa hiyo kupandisha bei ya bidhaa wakati mwingine mara mbili zaidi ya bei halisi.

Ili kuepukana na hilo ni muhimu kufanya manunuzi mapema hususan kwa bidhaa kama mavazi, vyakula visivyo vya kuoza na vinywaji ili kuepukana kuingia gharama kubwa na kupunguza msukumo (presha) ya kufanya manunuzi.

Ongeza vyanzo vya mapato

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanashauri ni vema kuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha mapato kwani chanzo kimoja pekee cha mapato wakati fulani huchangia ugumu hususani inapotokea dharura ambayo inaweza kuathiri bajeti ya awali.

Tovuti ya fikra za kitajiri inaeleza kuwa katika kila chanzo cha mapato ulichonacho ni muhimu kutenga kila mwezi asilimia fulani kwa ajili ya kufanikisha mahitaji ya ada au malipo ya pango la nyumba katika miezi ambayo fedha hizo zinatakiwa.

“Kama kuna uwezekano unaweza kuanzisha chanzo maalum kwa ajili ya kukamilisha kila hitaji la pesa. Endapo utatumia mbinu hii kwa nidhamu ikifika mwezi Januari unakuwa tayari umejiandaa kukamilisha mahitaji ya pesa kulingana na bajeti yako, “ inasema tovuti hiyo.

error: Content is protected !!