Mauzo ya nyama nje ya nchi kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 15 mwaka jana yalifikia tani 5,158.93 sawa na ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na tani 4,239.42 zilizouzwa kipindi kama hicho mwaka 2021 huku nchi ya Qatar ikiongoza kwa kununua tani 504.
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi alisema katika kipindi cha Novemba mwaka jana, Tanzania iliuza nje ya nchi tani za nyama 1,423 zenye thamani ya dola za Marekani 5,370,187.70 sawa na zaidi ya Sh bilioni 10 za Kitanzania.
Akizungumza wakati akitoa tathmini ya maendeleo ya uuzaji nyama nje ya nchi kwa Novemba mwaka jana, Dk Mushi, alisema kiasi hicho kilichouzwa ni sawa na ongezeko la asilimia 125, ikilinganishwa na tani 632 zilizouzwa Oktoba 2022.
“Tani 1,423 za nyama zilizouzwa Novemba mwaka 2022, ni sawa na ongezeko la asilimia 62 ikilinganishwa na tani 878 zilizouzwa Novemba mwaka 2021, mpaka hapo zimeongezeka tani 545,” alisema Dk Mushi.
Alisema mchanganuo wa tani hizo 1,423 za nyama zilizouzwa ni ya mbuzi tani 1,047, kondoo tani 343, ng’ombe tani 32, kuku tani 0.67 na nyama ya nguruwe tani 0.2.