Mfumuko wa bei washuka nchini

HomeKitaifa

Mfumuko wa bei washuka nchini

Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Disemba imeshuka kidogo baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo, ikichagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za vyakula.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Disemba  2022 umepungua kidogo hadi asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.9 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Novemba 2022.

Taarifa ya NBS iliyotolewa jana Disemba 10, 2022 inaeleza hali hiyo inamaanisha kupungua kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa.

“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba, 2022 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2022,” imesema taarifa ya NBS.

Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula ambazo mfumuko wa bei umeshuka ni pamoja na vifaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba ikiwemo saruji, mabati na bomba za maji kutoka asilimia 10.1 hadi asilimia 8.6 na nishati ya gesi kutoka asilimia 11.8 hadi asilimia 10.7.

Bidhaa nyingine ni mafuta ya taa kutoka asilimia 41.7 hadi asilimia 40.1,  nishati ya mkaa (kutoka asilimia -3.6 hadi asilimia -5.9) na samani kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 3.8.

Mfumuko wa dizeli umeshuka kutoka asilimia 28.4 hadi asilimia 27.4,  petroli (kutoka asilimia 9.5 hadi asilimia 3.7) na huduma ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya barabara mfano basi, taksi na pikipiki kutoka asilimia 7.9 hadi asilimia 6.3.

Miezi miwili ya kudumaa

Kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Disemba 2022 kumekuja baada ya kasi yake kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo.

Mwezi uliopita NBS ilieleza kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 ulikuwa asilimia 4.9 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Novemba 2022.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Licha ya mfumuko wa jumla kushuka, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka unaoishia Disemba 2022 umeongezeka kwa asilimia 0.2 kutoka ile iliyorekodiwa mwaka unaoishia mwezi Novemba mwaka jana.

Mfumuko huo wa bei kwa bidhaa vya vyakula umeongezeka kutoka asilimia 9.5 iliyorekodiwa Novemba 2022 hadi asilimia 9.7 mwaka unaoishia Disemba 2022.

error: Content is protected !!