Jamii ya Wahadzabe na Wadatoga wanaoishi wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha, wametishia kuyahama makazi yao kwa kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imetangaza tozo za utalii zinazopunguza maslahi yao.
Wamedai hawatatoa ushirikiano kwa mtalii yeyote atakayeingia kutembelea jamii yao na wamemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana aende kutatua mgogoro huo.
Walidai halmashauri imeamua kila mtalii anayeingia katika lango la Kijiji cha Qand’end kufanya shughuli za utalii ikiwamo kuiona jamii ya Wahadzabe, Wadatoga na Wahunzi alipe dola za Marekani 25 (58,400).
Ilidaiwa kuwa fedha hizo zikigawanywa, jamii hizo zinapewa dola za Marekani mbili tofauti na awali wakati kila gari la utalii lililipa dola za Marekani 110 (Sh 256,960) na jamii hizo zilipata dola za Marekani 20 (sh 46,720) kila moja.
Mwanakijiji Ntontowasi Nuika alidai Wahadzabe hawapo tayari kutumika kwa maslahi ya wengine wakati wao ni chanzo cha watalii kuingia kijijini hapo.
“Msimamo wetu iwapo serikali itashindwa kutusikiliza, hatutatoa ushirikiano kwa watalii tutahama maeneo haya, tumechoka kutumika kama karai la zege wakati sisi ndio kivutio cha watalii,” alidai mwanakijiji mwingine Kankono Thomas.