Afariki kwa kuangukiwa na jiwe akifanya adhabu baada ya kushindwa kuongea kiingereza

HomeKitaifa

Afariki kwa kuangukiwa na jiwe akifanya adhabu baada ya kushindwa kuongea kiingereza

Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia walimu wawili wa Shule ya Sekondari Mwinuko kwa kosa la kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha kwanza na mwingine kujeruhiwa waliokuwa wakitekeleza adhabu ya kusomba kifusi cha mchanga baada ya kuzungumza lugha ya Kiswahili shuleni.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mtafungwa akizungumza na waandishi wa habari jana Marchi 17, 2023 amesema tukio hilo limetokea jana saa 1:50 asubuhi ambapo wanafunzi hao wakiwa na wenzao 30 walipatiwa adhabu hiyo jana baada ya kuzungumza lugha ya Kiswahili shuleni kinyume na taratibu za shule hiyo.

Amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Gloria Faustine (14), mwanafunzi wa kidato cha kwanza huku  Emmanuel Lyatuu ambaye amajeruhiwa akiwa amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture akiendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda Mtafungwa amesema adhabu hiyo walipatiwa na mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalu Baluya ambapo walianza kutekeleza adhabu hiyo jana Machi 16 lakini hawakuimaliza hivyo leo wakawa wanaendelea nayo.

“Wakiwa wanaendelea kutekeleza adhabu hiyo, gafla jiwe kubwa lililokuwa linashikiliwa na udongo huo lilidondoka na kuwaangukia wanafunzi hao ambapo mmoja alifariki papo hapo na mwingine kujeruhiwa kwenye mguu wake wa kulia,” amesema Mtafungwa.

Amesema wanafunzi wengine waliokuwa kwenye adhabu hiyo walikimbia hivyo hawakuweza kupata madhara yoyote.

Amesema kitendo hicho kilizua taflani kwa wazazi wanaoishi eneo hilo ambapo walianza kuwashambulia walimu hao kwa kuwarushia mawe na kung’oa mbogamboga na viazi vilivyolimwa shuleni hapo.

Hata hivyo, vurugu  zilizuiwa na polisi na kufanikiwa kurejesha hali ya utulivu kwenye eneo hilo.

Kamanda Mtafungwa amesema wanawashikiliwa walimu hao kwa mahojiano zaidi kujua namna adhabu ilivyotekelezwa na usimamizi uliokuwepo wakati wanafunzi hao wakitekeleza lakini pia kujiridhisha udongo ulivyokuwa kwenye eneo hilo.

 “ Tunawashikilia walimu hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi kujua namna adhabu zilivyokuwa zimetolewa na namna walivyoweza kuzisimamia,” amesema Mtafungwa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Kamila Labani ametoa rai kwa walimu hususani katika kipindi hiki cha mvua kufahamu kuwa ardhi inakuwa oevu na watoto wanapenda kucheza kwenye mawe hayo wasiyaamini sana.

“Jiografia ya Mkoa wa Mwanza ni mawe, hivyo wazazi wasiyaamini sana hasa kipindi hiki cha mvua wawe waangalifu ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea,” amesema.

error: Content is protected !!