Rais Samia arejesha nyongeza za mishahara

HomeKitaifa

Rais Samia arejesha nyongeza za mishahara

Rais Samia Suluhu Hassan amerejesha utaratibu wa nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma ya kila mwaka ambao ulisitishwa kwa muda mrefu na ameahidi nyongeza hiyo itaanza kutolewa mwaka huu wa 2023.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Mei Mosi 2023 mkoani Morogoro katika sherehe za maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani amesema utaratibu huo utaanza mwaka huu.

 “Niseme pia kuna nyongeza za mishahara kwa mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa nikaona mwaka huu tuzirudishe.

“Kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu mbali niliyoyasema lakini kuna nyongeza za mishahara kila mwaka na tunaanza mwaka huu na tutaenda kila mwaka kama ilivyokuwa hapo zamani,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema Serikali haiwezi kutaja hadharani nyongeza hiyo ya mshahara ili kuepuka kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali sokoni kunakowezwa kufanywa na baadhi ya watu.

“Kile watu walichozoe tukisema hapa ili wapandishe bei madukani mara hii hakuna tunakwenda polepole kupandishana kama tulivyosema, wasione tumeongezeana kitu gani ili mwenendo wetu wa bei uwe salama,” amesema Rais Samia.

Amewataka wafanyakazi kutokuwa na wasiwasi kwa sababu “mambo mazuri yapo lakini hatutayatangaza hapa (kwenye sherehe za Mei Mosi) lakini wafanyakazi mambo ni moto, mambo ni fire.”

Rais Samia hajatangaza kupunguza kodi ya mishahara na kuongeza kima cha chini cha mishahara kama alivyofanya mwaka jana mpaka pale uchumi utakaporuhusu huku akiahidi kuboresha posho za wafanyakazi.

“Tulipandisha posho za wafanyakazi na waliofaidika na hili ni wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ambao hawakufaidika na asilimia 23 (nyongeza ya mshahara). Mwaka huu kuna mavuno makubwa upandishaji wa viwango vya posho vitapatikana,” amesisitiza Rais.

Akizungumzia kuhusu ukataji wa kodi ya marupurupu ya wafanyakazi, changamoto za bima ya afya, malimbikizo ya madeni ya mishahara na mafao ya  watumishi yaliyoibuliwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Heri Mkunda,  amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na watendaji wengine wa Serikali washughulikie ili ipatikane suluhu.

Licha ya changamoto lukuki za wafanyakazi, Rais Samia amewaahidi wafanyakazi kuendelea kuboresha mazingira na sheria za kazi ili kuhakikisha watumishi wa umma na sekta binafsi wanapata maslahi bora na kuboresha maisha yao.

error: Content is protected !!