Uzalishaji wa maziwa nchini umeongezeka kutoka lita bilioni 3.4 mwaka 2021/2022 hadi kufikia lita bilioni 3.6 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 5, Bunge limeambiwa.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
“Uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka mayai bilioni 4.9 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 5.5 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 12.2,” amesema Waziri Ulega na kuongeza:
“Vituo vya kukusanyia maziwa vimeongezeka kutoka 238 mwaka 2021/2022 vilivyokuwa vikikusanya lita milioni 11 64.8 kwa mwaka hadi kufikia vituo 246 mwaka 2022/2023 ambavyo vinakusanya takriban lita milioni 68.7 kwa mwaka.
“Aidha, viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 105 mwaka 2021/2022 vilivyokuwa vinasindika lita milioni 77.6 kwa mwaka hadi kufikia 152 mwaka 2022/2023 vinavyosindika lita milioni 77.3 kwa mwaka.
“Viwanda 47 vilivyoongezeka vina uwezo wa kusindika maziwa kati ya lita 100 hadi 1,000 kwa siku. Pia, katika kukidhi mahitaji ya soko la maziwa, vibali 605 vya kuingiza maziwa kutoka nje ya nchi vyenye jumla ya lita milioni 11.6 zenye thamani ya shilingi 22,765,482,217.50 vilitolewa,” amesema Waziri Ulega.