Rais Samia kushiriki tamasha la utamaduni, Mwanza

HomeKitaifa

Rais Samia kushiriki tamasha la utamaduni, Mwanza

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara kikazi mkoani Mwanza kwa siku tatu ambapo atashiriki uzinduzi wa tamasha la Bulabo pamoja na kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.

Bulabo ni tamasha la utamaduni la wasukuma ambalo hufanyika kila mwaka msimu wa mavuno unapowadia ambapo huandaliwa na kituo cha utamaduni cha Bujora pamoja na Watemi wa koo mbalimbali za kisukuma ambapo kwa mwaka 2023 litafanyika Kisesa katika Wilaya ya Magu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla aliyekuwa akizungumza na wakuu wa taasisi zinazosimamia miradi ya mkakati jana Juni 8 2023, amewaambia Rais Samia atawasili Juni 12 ambapo Juni 13 atazindua tamasha hilo na Juni 14 atatembelea miradi.

“Chifu Hangaya anarudi kule alipopewa uchifu, hivyo tutakuwa na tamasha kubwa, maandalizi yanaendelea na yapo katika hatua nzuri. Juni 14 katika Mkoa wetu Rais atapita katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kufuatilia mradi wa Kigongo-Busisi, mradi wa ujenzi wa meli ya Mv Mwanza pamoja na hoteli ya NSSF,” amesema Makalla.

Septemba 8, 2021 Rais Samia alisimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Tanzania Mkoani Mwanza wakati akifunga Tamasha la Utamaduni lililoandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania.

RAIS SAMIA AAPISHWA KUWA CHIFU MKUU WA MACHIFU TANZANIA, APEWA JINA  'HANGAYA'

Pamoja na kutawazwa kuwa Chifu Mkuu wa Machifu wote nchini, Rais Samia alipewa  jina la Chifu Hangaya likiwa na maana ya Nyota ya asubuhi inayong’aa.

Kwa mujibu wa Rais Samia Utamaduni hutangaza mila na desturi za nchi lakini pia ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwasababu ni moja ya vivutio vya utalii.

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2023/24 imepanga kuboresha utalii wa utamaduni pamoja na matarajio ya kupata jumla ya watalii 63,519 na mapato ya wastani wa Sh265.5 milioni.

Pamoja na kushiriki katika uzinduzi wa tamasha hilo Rais Samia atatembelea baadhi ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Mwanza ya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

error: Content is protected !!