Wanaume nchini wameshauriwa kutovumilia na kuficha vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwenye ndoa na kwenye familia zao.
Badala yake, wametakiwa kutoa taarifa katika vyombo vya kupinga unyanyasaji huo ikiwamo Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi.
Pia wameelekezwa kupeleka malalamiko yao kwenye Ofisi za Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mtendaji Kata na Mtaa ili kuepukana na athari za vitendo hivyo.
Wito huo ulitolewa katika maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani na Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (Smaujata) Mkoa wa Mwanza, Gasto Didas.
Alisema uwepo wa madawati ya kijinsia nchini ni kuona usawa na ustawi kwenye jamii ili kuepusha vitendo hivyo ambapo ukatili haufanywi kwa wanawake na watoto pekee bali hata kwa wanaume lakini wengi wao wamekuwa wakikaa kimya.
“Ni kweli kwamba sisi wanaume tumekuwa wasiri sana hususani kwa kuhisi utaonekana mdhaifu kumbe ndio unajiongezea matatizo ya kisaikolojia,” alisema.
Didas alisema kwa sasa wanaume wengi wanafanyiwa ukatili wa kisaikolojia ambao kwa kiasi kikubwa umewasababishia msongo wa mawazo na baadhi kutokuwa na furaha na familia zao.