Wanafunzi 150 kutoka Sudan wahamishiwa Muhimbili

HomeKitaifa

Wanafunzi 150 kutoka Sudan wahamishiwa Muhimbili

Wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum nchini Sudan wamehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuwakaribisha wanafunzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa hali ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Sudani imesababisha kufungwa kwa vyuo na baadhi ya shughuli kusimama hivyo watalamu hao kushindwa kuendelea na ratiba yao ya masomo ya kawaida.

“Wanafunzi hawa wapo mwaka wa tano wa shahada ya kwanza ya utabibu, ambapo katika mwaka huo, mafunzo hufanyika kwa vitendo zaidi, hivyo madaktari hawa wanafunzi watafanya mzunguko (Rotation) katika idara mbalimbali ikiwemo idara ya upasuaji chini ya usimamizi wa madaktari bingwa ili kuhakikisha wanapata maarifa yanayotakiwa” amesema Prof. Janabi.

Amebainisha kuwa MNH itatoa fursa kwa wataalamu hao kujifunza kama ambavyo inatoa kwa wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi na hata baada ya kumaliza masomo kama watapenda kufanya mafunzo tarajali (Intenship) MNH itawapa nafasi hiyo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo cha UMST, Prof. Mamoun Homeida amesema kuwa amefurahi kuona wanafunzi kutoka chuo anachokisimamia wamepokelewa vizuri na kwamba jambo hili limetokana na mahusiano ya kindugu yaliyopo baina na Tanzania na Sudan.

Kwa upande wake Bi. Ruba Anwar Salih ambaye ni kiongozi wa kundi la wanafunzi hao amesema kuwa wamefurahi kupata fursa ya kuendelea na masomo katika Hospitali kubwa na yenye wataalamu wa kutosha, ni imani yao kwamba watapata fursa nzuri ya kujifunza.

error: Content is protected !!