Rais Samia Suluhu Hassan amesema amevutiwa zaidi na ramani ya Uwanja wa Mashujaa, Dodoma ambapo jambo la kipekee na kubwa zaidi katika ramni hiyo ni ujenzi wa mnara mrefu zaidi Afrika katika Uwanja huo uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba.
Rais Samia amesema hayo wakati akishiriki maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa katika Uwanja wa Mashujaa.
“Nilipofika nilioneshwa ramani uwanja utakavyokuwa nimevutiwa sana na ramani ya uwanja wa Mashujaa, uwanja huu utakuwa na migahawa ya Kimataifa, kumbi za mikutano na vivutio vingine vya Watu kupumzika (…) utakuwa na mnara mrefu kabisa ndani ya Afrika yetu.” alisema Rais Samia.
Aidha, akihitisha hotuba yake Rais Samia amewataka Watanzania kuendelea kushikamano, kuwa na utulivu, umoja na upendo kama njia moja wapo ya kuwaenzi mashujaa wetu huku akisisitiza kutokubaliwa kugawanywa na mtu au kundi lolote lile.
“Kamwe, kamwe tusikubali mtu yeyote au kikundi cha watu kutugawa kwa kisingizio chochote kile. Tanzania ni moja na kamwe haitagawanyika.” amesema Rais Samia.