Rais Samia Suluhu Hassan amesema njia pekee ya kuwa na vijana watakaosaidia kulijenga taifa lenye maendeleo kwa siku za mbeleni ni kuwekeza kwenye mtaji wa elimu na serikali yake imeshaanza uwekezaji huo na itaendelea kuwekeza.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 26, 2023 katika mkutano wa wakuu wanchi za Afrika kuhusu rasilimali watu unaoendelea katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julias Nyerere Dar es Salaam.
“Tupo tayari kuwekeza kwenye elimu na tumeanza na elimu ya awali ambapo elimu ya awali zamani ilikuwa ni kama sehemu wachimba madini, wakulima wanaweka tu vibanda ili watoto wao wasome pale ,lakini kama serikali tumejenga shule za kisasa kabisa ambazo watoto wale wanasoma.
Na ni watoto kuanzia miaka miwili mpaka miaka mitano kwa sababu miaka sita wanaanza elimu ya msingi.”amesema Rais Samia
Rais Samia ameongeza kuwa serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza kwenye shule za msingi ikizingatiwa kwamba idadi ya watu Tanzania ni kubwa na inakuwa kwa kasi hivyo kila mwaka wanatumia fedha nyingi kujenga shule za msingi pamoja na Sekondari lakini pia kuwekeza katika elimu ya juu.