Serikali inavyokabiliana na changamoto za masoko ya bidhaa za kilimo

HomeKitaifa

Serikali inavyokabiliana na changamoto za masoko ya bidhaa za kilimo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake inatekeleza mikakati madhubuti kukabiliana na changamoto ya uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo yanayozalishwa nchini, ikiwemo kusaidia tafiti za mazao yenye uhitaji na kuwaunganisha wakulima na masoko.

Hatua hiyo huenda ikachochea uzalishaji wa mazao na kuongeza kipato kwa wakulima, jambo litakalokuza uchumi wa nchi pamoja na kupaisha mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, mwaka 2022 sekta hiyo ilichangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, kutoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na vijana katika mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRAF) leo Septemba 7, 2023, amekiri kuwa kuna changamoto ya soko nchini na tayari wameshafanya utafiti na kubaini namna ya kukabiliana nayo.

“La kwanza ni kubaini bidhaa gani inatakiwa wapi, ndani na nje ya nchi, tukijua hilo tunakuwa na hakika kinachozalishwa kiende wapi, la pili ni kuwaunganisha wakulima na soko lenyewe, hapa bado hatujafanya vizuri,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.

Rais Samia ameongeza kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha wakulima wanakutana na wanunuzi moja kwa moja tofauti na sasa ambapo katika baadhi ya maeneo wakulima hulazimika kuuza mazao yao kwa walanguzi ambao hununua kwa bei ya chini.

Kulitekeleza hilo, Rais Samia amesema wamewashawishi wakulima kuuza mazao yao kwa kutumia vyama vya ushirika ambako huuza kwa bei ya ushindani akitolea mifano zao la mbaazi lililouzwa hivi karibuni kwa bei ya juu.

“Mbaazi ilianguka sana bei na kuwavunja moyo wakulima, mwaka jana iliuzwa Sh300 kwa kilogramu moja, mwaka huu wakulima wameuza kwa Sh2,000 na kuendelea, huu ndio mtindo tutakaoenda nao kwenye mazao mengine,” ameongeza Rais Samia.

Miundombinu yatajwa

Hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara zinazounganisha wilaya na mikoa pamoja na zile zinazounganisha nchi jirani ili mazao yafike kwenye masoko kwa wakati.

Kununuliwa kwa ndege ya mizigo pamoja na upanuzi wa bandari ni miongoni mwa jitihada zinazotajwa kuchochea usafirishaji wa mazao kwenda nje ya nchi.

“Pale bandarini tunajenga kituo cha kuhifadhi mazao yanayoharibika haraka, yaweze kuhifadhiwa wakati yanasubiri usafiri, tunachukua hatua zote hizi ili kumfikisha mkulima kwenye soko,” amesema Rais Samia.

Sambamba na hayo, Rais Samia ametumia jukwaa hilo kutoa rai kwa viongozi mbalimbali walioshiriki mkutano huo kuwasikiliza zaidi vijana ili waweze kubaini ni changamoto gani zinazowakwamisha kushiriki kwenye sekta ya kilimo na namna gani ya kuzikwamua.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) asilimia 70 ya watu walioko kusini mwa jangwa la Sahara ni vijana walio na umri wa miaka 30.

Idadi hiyo inaweza kutumika vyema kuongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na kuinua uchumi wa mataifa hayo ya Afrika.

 

error: Content is protected !!