Na Faustine Kapama-Mahakama
Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kumuongezea muda Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hauvunji Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.
Hii ni kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, uliotolewa jana tarehe 22 Septemba, 2023, na kutupilia mbali kesi ya kikatiba lililowasilishwa na Humphrey Malenga, mleta maombi, ambaye ni raia wa kawaida.
“Rais ana mamlaka kwa mujibu wa Ibara ya 120 (3) inayosomwa pamoja na Ibara ya 118 (2) ya Katiba ya kuongeza muda wa Jaji wa Rufani ili kumwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yake. Naona maombi hayana mashiko. Nayatupiliwa mbali,” Jaji Godfrey Isaya alisema.
Katika maombi yake, mleta maombi alitaka amri ya kutafsiri masharti ya Ibara ya 118 (2) ya Katiba kuhusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu kuwa miaka 65 na si umri wa kustaafu kwa Jaji wa Rufani.
Pia alitaka tafsiri ya kifungu hicho kuwa ni Ibara inayosimama pekee na haihusanishwi na masharti ya Ibara ya 120 (1) (2) (3) na (4) ya Katiba wakati wa kuamua muda au umri wa kustaafu kwa Jaji Mkuu.
Aidha, mwombaji aliomba tafsiri ya mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusimamisha umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani au kuongeza muda wa utumishi wa Jaji wa Rufani kwa maslahi ya umma kwa mujibu wa Ibara ya 120 (2) na (3) haimhusu Jaji wa Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu.
Alitaka pia tamko kwamba kusimamishwa kwa umri wa kustaafu au kuongeza muda wa kukaa kwa Jaji wa sasa wa Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa mujibu wa kifungu cha 120 (2) na (30) ni kinyume cha Katiba.
Katika hukumu yake, Jaji Isaya alisema kuwa Ibara ya 118 ya Katiba haiwezi kusomwa peke yake, bali inasomwa pamoja na Ibara ya 120 ya Katiba, hivyo mamlaka ya Rais kuongeza muda wa Jaji Mkuu wa sasa madarakani yalikuwa sahihi, hivyo yako sambamba na Katiba.
“Ibara ya 120 (1) haiwezi kusomwa kipekee na Ibara ya 120 (2) (3) na (4), kwa maana hiyo kifungu cha 120 cha Katiba kinamhusu Jaji Mkuu, kusimamisha kwa usahihi umri wa kustaafu au kuongeza muda wa Jaji wa Rufani ambaye ni Jaji Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 120 (2) na (3) ni halali,” alisema.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Isaya alizingatia baadhi ya hoja kadhaa, ikiemo iwapo Masharti ya Ibara ya 118(2) ya Katiba yanaruhusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu kuwa miaka 65 au umri wa kustaafu wa Jaji wa Rufani.
Jaji pia alizingatia iwapo Ibara ya 118(2) ya Katiba ni Ibara ya “kusimama peke yake” wakati wa kuamua umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, au iwe katika kuamua umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu wa Tanzania kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 118(2) ya Katiba inafanyiwa rejea kwenye Ibara ya 120(1) pekee na kutukuzingatia masharti ya Ibara ya 120(2), (3) na (4) ya Katiba.
Pia ilizingatiwa iwapo mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusimamisha umri wa kustaafu kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani au kuongeza muda wa utumishi wa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa maslahi ya umma kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 120 (2) na ( 3) ya Katiba ni sahihi.
Aidha, Jaji alizingatia iwapo kusimamishwa kwa umri wa kustaafu na/au kuongeza muda wa kukaa kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye ni Jaji Mkuu kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 120(2) na, au 120(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. ya Tanzania kama ilivyofanyiwa marekebisho.
Katika kuamua hoja hizo, Jaji Isaya alieleza kuwa ni kweli maneno ya Ibara ya 118(2) yametungwa kwa namna ambayo inamlazimu mtumishi wa ofisi ya Jaji Mkuu kufanya kazi za utawala na Mahakama.
Alipata mantiki katika kutafsiri kwamba vifungu vilivyotajwa vinaunganisha ofisi ya Jaji Mkuu na Jaji wa Rufani pamoja na kukubaliana na mwombaji kwamba mwenye nafasi ya ofisi ya Jaji Mkuu pia ni Jaji wa Rufani.
“Sikubaliani na maoni ya mleta maombi kwamba kuna hatari na uvunjifu mkubwa wa Katiba. Kabla ya kuteuliwa katika ofisi ya Jaji Mkuu, Jaji Mkuu aliyeko madarakani alikuwa Jaji wa Rufani,” alisema.
Jaji Isaya aliuliza swali iwapo ibara ya 118 (2) ya Katiba inajitosheleza yenyewe ndani ya Katiba. Alisema kuwa jibu la swali hilo ni hasi kwa sababu pande zote mbili zinakubaliana kwamba umri unaotarajiwa wa kustaafu wa Jaji wa Rufani ni kama ilivyoainishwa chini ya Ibara ya 120(1) ya Katiba.
“Hii ina maana, ili kupata umri wa kustaafu kwa Jaji Mkuu inabidi kufanya marejeo ya Ibara ya 120(1) ya Katiba. Hii ni kwa sababu Ibara ya 118(2) ya Katiba haiwezi kusimama yenyewe peke yake au inaweza kujitosheleza….
“Nina hakika kwamba Ibara ya 120 (1) inahusiana na inafanya kazi kwa kuzingatia masharti ya Ibara iliyofuata. Hakika, hakuna katazo kwa Rais kila anapoona ni kwa manufaa ya umma kwamba Jaji wa Rufani kuendelea kuwa madarakani baada ya kufikisha umri wa miaka 65 chini ya Ibara ya 120 (3) ya Katiba. Kwa kuwa ni sehemu muhimu ya Jaji wa Rufani, Jaji Mkuu naye pia anahusika,” alisema.