Rais Samia ampa miezi sita Mkurugenzi mpya wa Tanesco

HomeKitaifa

Rais Samia ampa miezi sita Mkurugenzi mpya wa Tanesco

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukomesha mgao wa umeme unaoendelea kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza baada ya hafla ya kuwaapisha viongozi wateule leo, Septemba 26, 2023, amemwambia Boniface Nyamo-Hanga, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco kuwa kazi yake ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa miundombinu ili kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme.

“Nakupa miezi sita, nakuangalia pale Tanesco, kazi yako ya kwanza kusimamia ukarabati wa mitambo, baada ya miezi sita nisisikie kelele za kukatika kwa umeme, tutasaidiana nenda najua unaweza,” amesema Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.

Septemba 23, 2023 Rais Samia alimuondoa Maharage Chande kuwa Mkurugenzi wa Tanesco na kumteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kabla ya kumhamisha tena kuwa Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania siku mbili baadaye.

Ndani ya mwezi mmoja kumekuwa na malalamiko lukuki kutoka kwa watumiaji wa umeme kutokana na mgao wa umeme unaoendelea ambao Maharage alisema unatokana na upungufu wa nishati hiyo kutokana na ukame.

Chande ameondoka Tanesco na Mwenyekiti wa bodi hiyo baada Rais Samia kumteua Meja Jenerali Paul Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo akichukua nafasi ya Omar Issa anayeendelea na majukumu mengine ya Ofisi Rais-Tume ya Mipango.

Kuondolewa kwa viongozi wa juu wa Tanesco kumekuwa kukihusishwa na baadhi ya wachambuzi na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini na mgao unaoendelea lakini leo Rais Samia amesema tatizo hilo si la Chande pekee bali la Taifa.

Kwa mujibu wa Rais Samia uhaba wa umeme uliopo nchini hivi sasa umechagizwa na mabadiliko ya tabianchi, ubovu wa mitambo ya umeme pamoja na upungufu wa maji katika vyanzo vya umeme.

Rais Samia amesema tayari Serikali imeshachukua hatua kukabiliana nayo ikiwemo kukarabati mitambo, kujenga vituo vya kupoozea umeme na kuiunganisha baadhi ya mikoa na gridi ya taifa.

error: Content is protected !!