Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameliagiza Shirika la Ndege la Air Tanzania kuimarisha utoaji wa taarifa kwa wateja wao ili kuepusha sintofahamu pindi ndege zinapoahirishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 02,2023, Waziri Mbarawa alikiri kuwepo kwa changamoto kwenye kitengo cha utoaji taarifa katika shirika hilo la ndege na kusema hatua zichukuliwe kutatua hadha hiyo.
“Ndege inaweza kuchelewa lakini jinsi gani unavyomueleza mteja wako hiyo ni muhimu…Tanzania watu wengi wanaipenda Air Tanzania na wanataka wasafiri na Air Tanzania lakini na sisi tuliopewa dhamana lazima tukatoe huduma nzuri
“Ukimpa meseji ndege inachelewa masaa saba unampa meseji saa kumi na mbili jioni sio sahihi lazima tukubali” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof Mbarawa amesema ujio wa ndege mpya ya Boeing 737 Max 9 kesho itasaidia kupunguza changamoto hiyo.