Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itautizama upya na kubadili mfumo wa sasa wa uteuzi wa mabalozi, ili kurejesha hadhi, umahiri na ubobevu wa Tanzania katika medani za diplomasia.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amebainisha kuwa utaratibu wa sasa unahusisha hata watu ambao hawana vigezo vya kufanya kazi hiyo.
“Tunavyofanya sasa, wizara inaleta mapendekezo, sijui kama kuna vigezo au la, wakati huo nami mkononi nina mengine, nani kachafua wapi atoke na tunampeleka ubalozini…
…Lazima tuliangalie vizuri, sasa hivi anayevurunda kazini akae pembeni, tufumbe macho, hakuna kumpoza,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameongeza kuwa wakati mwingine uhusiano wa karibu na kindugu baina ya watendaji katika Wizara ya Mambo ya Nje ulikuwa chanzo cha watu kupangiwa majukumu ya kibalozi hata kama hawastahili.
Hata hivyo, Balozi Yahya Simba, Mwenyekiti wa Kamati ya Kutathmini Utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ambaye alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo alibainisha kuwa miongoni mwa mambo waliyobaini ni uwepo wa tuhuma za uwepo wa upendeleo kwa misingi ya undugu au ukabila wakati wa utoaji na upangaji wa baadhi ya ajira.
Balozi Simba ameongeza kuwa jambo hilo limechangia kushusha weledi na morali ya watumishi wa wizara na wizara kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Rais Samia uwepo wa makandokando na shutuma kwa Wizara ya Mambo ya Nje ni miongoni mwa mambo yaliyomsukuma kuunda kamati ya kutathmini utendaji kazi wake ili kuchechemua diplomasia ya Tanzania iliyodorola kutokana na kupungua kwa ufanisi wa wizara hiyo.
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na kamati kushughulikiwa na Serikali ni pamoja na, kuunda wizara ya kushughulikia mambo ya Afrika Mashariki pekee, kubadili jina la wizara, kuimarisha rasilimali watu na miundombinu ya wizara, na kuhamasisha matumizi ya Tehama.
Mapendekezo mengine ni kukuza vipaji pamoja na mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi, kuweka vipimo vya utendaji na kuiweka chini ya Ofisi ya Rais.
Hata hivyo Rais Samia amesema baadhi ya mapendekezo yatafanyiwa kazi mara moja ikiwemo kulea vipaji na mafunzo ya diplomasia kwa baadhi ya Watanzania huku mengine yakitakiwa kusubiri kwa muda.