Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejidhatiti katika kuhakikisha kwamba wilaya nchini kuna chuo cha ufundi huku lengo likiwa ni kuandaa nguvukazi inayohitajika katika uzalishaji na uongezaji wa tija katika shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.
Amesema hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Samora wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
“Tumeamua wilaya zote za Tanzania hii ziwe na vyuo vya aina hii lakini mbali na wilaya kuwe na chuo cha mkoa kila mkoa. Lengo ni kujenga vyuo ambavyo vinakwenda kufundisha elimu ya amali kwa vijana wetu na sio nadharia wanazopata shuleni.” amesema Rais Samia.
Ikiwa leo ni siku yake ya kwanza ya ziara mkoani Tabora, Rais Samia aliwaambia wananchi kwamba serikali imedhamiria kukuza ujuzi wa vijana kwa sababu ndio nguvu kazi ya taifa.
Rais Samia amezindua leo Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Igunga- Tabora kilichojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 huku kikitarajiwa kuhudumia wanafunzi 900.
Aidha, Rais Samia amewasihi wananchi wa Tabora kuchangamkia fursa zilizopo katika mkoa huo ili waweze kunufaika nazo.