Mabadiliko katika miundombinu, teknolojia ya kupakua na kupakia shehena na kasi ya kuhudumia meli katika Bandari ya Dar es Salaam kumeifanya bandari hiyo kuendelea kuaminika, hivyo kupokea meli nyingi zenye ukubwa stahiki katika biashara ya bandari.
Aidha katika mwaka huu wa fedha 2023/24 bandari hiyo imevuka lengo la nusu ya kwanza kwa kushughulikia shehena ya tani milioni 12 kati ya lengo walilopangiwa la tani milioni 22 kwa mwaka. Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho wakati wa kufanya majumuisho na waandishi wa habari ambao walitumia zaidi ya saa mbili kutembelea bandari hiyo yenye gati 12.
Alisema pamoja na kwamba walipangiwa lengo la serikali la tani milioni 22 wao bandari wamepanga lengo la kuhudumia shehena ya tani milioni 24 na wanahakika watalivuka lengo hilo kutokana na mipango yao na pia kuwapo kwa ufanisi katika uhudumiaji wa meli.