Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.4 (karibu Shilingi trilioni 4) ndani ya miezi mitatu ya mwisho ya mwaka jana.
Hili ni ongezeko la asilimia 80 kulinganisha na miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 769.6 iliyosajiliwa kwenye kipindi kama hicho kilichopita (Oktoba-Desemba 2022).
Ongezeko hilo kubwa la uwekezaji limetokana na ziara za nje za Rais Samia Suluhu Hassan za kuvutia wawekezaji kupitia diplomasia ya uchumi na kuimarishwa kwa mazingira ya biashara nchini ambayo yamevutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani.
Rais Samia amekuwa akisafiri nchi mbalimbali duniani akiambatana na wafanyabiashara wa Tanzania ili kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na mataifa ya nje.
Ripoti mpya ya TIC inaonesha kuwa jumla ya miradi 161 ilisajiliwa kwenye kipindi cha Oktoba-Desemba 2023 ikilinganishwa na miradi 58 kwenye kipindi kama hicho mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 178.
Sekta tano zilizo ongoza kwenye uwekezaji huo ni viwanda (Dola milioni 690.8), usafirishaji (Dola milioni 241.8), huduma (Dola milioni 122.5), kilimo (Dola milioni 89.1) na utalii (Dola milioni 83.3).
Miradi iliyosajiliwa Oktoba-Desemba 2023 inatarajiwa kutengeneza jumla ya ajira mpya 18,390, kutoka ajira 10,216 za kipindi kama hicho kilichopita kwa mwaka 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, amesema kuwa kituo hicho kimeanzisha kampeni maalumu ya kukuza uwekezaji wa ndani.
“Lengo letu ni kusajili miradi ya uwekezaji wa ndani yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 (Shilingi trilioni 9) hadi ifikapo mwaka 2028,” Teri amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za TIC, mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imeongoza kwa kupata uwekezaji mkubwa zaidi nchini kwenye miezi mitatu ya mwisho ya mwaka jana.
Dar es Salaam iliweza kuvutia miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 454.7, wakati mkoa wa Pwani ulipata miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 380.7.