Sera za uchumi za Rais Samia zaleta neema kwa mabenki

HomeKitaifa

Sera za uchumi za Rais Samia zaleta neema kwa mabenki

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Sera nzuri za uchumi za serikali tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani zimeleta neema kubwa kwenye sekta ya benki nchini, huku benki za biashara zikivunja rekodi ya mapato na faida mwaka jana.

Faida kubwa ambazo benki zimepata nchini kutokana na uchumi tulivu na unaokuwa kwa kasi tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 2021, zimeziwezesha kufungua matawi mengi zaidi nchini na kumwaga ajira kwa Watanzania.

Benki hizo pia zimeongeza idadi na ukubwa wa mikopo zinazotoa kwa sekta binafsi na kuchochea zaidi ukuaji wa uchumi.

Ongezeko kubwa la faida kwa benki hizo limezifanya zilipe kodi kubwa zaidi kwa serikali na gawio kubwa zaidi kwa zile benki ambazo serikali inamiliki hisa.

Taarifa za robo ya nne ya mwaka (Oktoba-Desemba 2023) za mabenki ambazo zimechapishwa jana zinaonesha kuwa benki mbili kubwa nchini – CRDB na NMB – zinaendelea kuwa vinara wa sekta ya fedha nchini.

Benki ya NMB imevunja rekodi nchini kwa kupata faida ghafi (gross profit) ya Shilingi bilioni 775 kwenye kipindi cha mwaka mmoja kinachoishia Desemba 31, 2023.

Benki hiyo pia ilifungua matawi mapya manne na kuajiri wafanyakazi wapya 98 mwaka jana.

Hii imeongeza jumla ya wafanyakazi wa NMB kufikia 3,642 na jumla ya matawi yake kuwa 231.

Kutokana na mazingira mazuri ya uchumi nchini tangu Samia awe Rais, NMB iliongeza kiasi cha mikopo inayotoa kwa asilimia 28, hadi kufikia Shilingi trilioni 7.7 mwaka jana.

Kwa upande wa CRDB, benki hiyo ilipata faida ghafi ya Shilingi bilioni 599 mwaka jana.

CRDB pia iliongeza jumla ya mali (total assets) zake hadi kufikia Shilingi trilioni 13.2, wakati amana za wateja (customer deposits) ziliongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 8.8.

Kutokana na uchumi wa Tanzania kukuwa kwa kasi chini ya Rais Samia, Benki ya CRDB mwaka jana iliongeza kiasi cha mikopo inayotoa hadi kufikia Shilingi trilioni 8.8.

Ukuaji wa kasi wa uchumi nchini umeiwezesha CRDB kufungua mawawi 10 mapya nchini mwaka jana na kuajiri wafanyakazi wapya 232.

Benki za biashara zinatarajiwa kuweka rekodi mpya ya faida mwaka huu mpya wa 2024 na kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi kutokana na mazingira mazuri ya uchumi na uwekezaji chini ya serikali ya Awamu ya 6 ya Rais Samia.

error: Content is protected !!