Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kwa asilimia 100 ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Songwe huku ikiendelea na kazi ya upanuzi wa barabara ya njia nne kuanzia Uyole (Nsalaga) hadi Ifisi km 29 katika barabara kuu ya TANZAM.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya Mha. Masige Matari amesema hayo tarehe 21 Machi 2024 alipozungumza na kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita Chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Ujenzi wa barabara, Madaraja na viwanja vya Ndege.
Amesema kwa asilimia 100 Mkandarasi China Geo- Engineering Corporation ya China amekamilisha kazi ya upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege; ambapo pia Mkandarasi GECI Espanola S.A wa Spain naye amekamilisha kazi zote za kusimika miundombinu ya taa katika njia ya kuruka na kutua ndege.
Amebainisha kuwa ujenzi wa njia nne unaotekelezwa na Mkandarasi M/s China Henan International Cooperation Group Co.Ltd (CHICO) unagharimu shilingi bilioni 138.727 na maboresho katika uwanja wa ndege wa Songwe ikihusisha ujenzi wa jengo jipya, kusimika miundombinu ya na barabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa zaidi ya km 3 imegharimu jumla ya shilingi bilioni 33. 564.
Pia Serikali imekamilisha matengenezo katika eneo la Inyala ambayo yamehusisha ujenzi wa barabara ya mchepuo kwa kiwango cha lami yenye kilometa 2.8, kupanua barabara kuu kutoka mita 6.7 kwenda 10.5 kutengeneza maeneo matatu ya dharura ya kutoa magari barabarani na kuweka taa katika maeneo mawili ya Inyala na Shamwengo kwa gharama ya shilingi bilioni 6.999.
Mha. Matari amesema mradi wa barabara ya Igawa – Tunduma km 218 na Uyole – Songwe (Bypass) km 48.9 unajengwa kwa utaratibu wa EPC + F kwa gharama ya shilingi trilioni 1.133 ambazo ni fedha za Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Aidha ujenzi wa barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu km 81 kwa kiwango cha lami; Sehemu ya Bujesi – Mbambo km 10 na Tukuyu – Mbambo km 7 unaendelea na tayari usanifu na upembuzi yakinifu umekamilika katika ujenzi wa barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete km 96.2