Kazi Iendelee: Rais Samia azindua safari ya treni ya kisasa ya SGR

HomeKitaifa

Kazi Iendelee: Rais Samia azindua safari ya treni ya kisasa ya SGR

Dar es Salaam, Tanzania – Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi safari ya treni ya kisasa ya SGR (Standard Gauge Railway) leo, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inakamilika kwa viwango na ubora uliokusudiwa.

Katika hotuba yake, Rais Samia alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu, akisema, “Katika kipindi hiki cha miaka mitatu safari hii ya maendeleo tumekwenda nayo haraka sana. Kwahiyo tunaposema kazi iendelee, maana yake kazi iendelee.” Alisisitiza kwamba dhamira yake ni kuendeleza miradi iliyokuwa imeanzishwa katika awamu ya tano chini ya uongozi wa Hayati Rais John Pombe Magufuli.

Rais Samia aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa viongozi, watendaji, wakandarasi na wananchi kwa ujumla, sasa mradi wa SGR umefikia hatua ya kutekelezwa, akisema, “Leo tunaweza kusema mradi wa SGR sio ndoto tena bali ni uhalisia.”

Akielezea umuhimu wa mradi huu, Rais Samia alisema, “Miundombinu imara ya usafiri ni kichocheo muhimu sana cha ukuaji wa uchumi. Tafiti zinaonyesha kuwa kukosekana kwa miundo imara ya usafiri kunashusha pato la nchi za Afrika kwa wastani wa asilimia 2 na kuongeza gharama za usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 40.”

Kupitia mradi huu wa SGR, muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma umepunguzwa kwa asilimia 60, kutoka masaa tisa hadi wastani wa saa tatu na nusu. Hatua hii, kwa mujibu wa Rais, itarahisisha shughuli za kibiashara na kijamii kati ya majiji haya mawili muhimu nchini.

Rais Samia alibainisha pia kwamba mradi wa SGR utapunguza msongamano wa magari barabarani, kupunguza ajali, na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo. Aidha, mradi huu unatarajiwa kuchangia katika kupunguza uharibifu wa mazingira na kuchochea shughuli za kiuchumi katika sekta za viwanda, kilimo, ufugaji, utalii, na biashara.

“Mradi huu vilevile utachochea ukuaji wa sekta ya viwanda katika maeneo mengi ya nchi kutokana na uhakika wa usafiri na usafirishaji,” alisema Rais Samia, akiongeza kuwa uendeshaji wa reli hii ya kisasa utatoa fursa za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini na kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa kauli yake ya “Kazi Iendelee,” Rais Samia amedhihirisha dhamira yake ya kuendeleza na kukamilisha miradi yote ya kimkakati nchini Tanzania.

error: Content is protected !!