Marais wa Afrika kupakiwa kwenye basi ni dhihaka?

HomeKimataifa

Marais wa Afrika kupakiwa kwenye basi ni dhihaka?

Na Abbas Mwalimu

(0719258484).

Jumatatu tarehe 19 Septemba, 2022.

Kumekuwa na mijadala mingi kuhusu viongozi  wa Afrika kupakiwa kwenye usafiri (bus) wa gari moja wakati wakielekea kwenye ibada ya mazishi Westminster Abbey.

Swali ni je walikuwa viongozi wa nchi za Afrika pekee?

Kwa nini matukio makubwa au mikutano hutumia mabasi?

Kimsingi hawakuwa viongozi wa Afrika pekee waliopanda kwenye mabasi bali viongozi wengi walioalikwa walitumia mabasi.

Tukumbuke kuwa tukio lile lilikutanisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali na Wawakilishi zaidi ya 500 kutoka nchi na taasisi mbalimbali duniani hivyo maandalizi ya usafiri yalihitaji kuratibiwa vizuri.

Kimsingi baadhi ya viongozi waliopanda mabasi ni Waziri Mkuu wa Ireland Micheál Martin, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, Waziri  Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern, Mfalme Abdullah II wa Jordan na mkewe Malkia Rania.

Aidha wengine waliopanda mabasi ni Rais wa Malaysia Agong Al-Mustafa Billah Shah, Rais wa Singapore Halimah Yacob, Mfalme wa Japan Naruhito, Rais wa Poland Andrzej Duda, na Rais wa Ujerumani  Frank-Walter Steinmeier.

Vilevile, Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden na mkewe Silvia, Malkia Margrethe II wa Denmark, Mfalme Felipe na Malkia Letizia wa Hispania, Rais wa Italia Sergio Mattarella, Rais wa Umoja wa Ulaya  Ursula von der Leyen, Mfalme Harald wa Norway na mkewe Malkia Sonja nao walipanda mabasi.

Matukio makubwa kama mikutano au msiba kama ule wa Malkia Elizabeth II ambao ulikutanisha viongozi wengi njia rahisi ya kuwafikisha katika tukio kwa muda uliopangwa ni kutumia usafiri wa pamoja.

Tufahamu kuwa matukio ya namna ile yanaongozwa na itifaki (protocol) na miongoni mwa mambo muhimu katika protocol ni muda.

Sasa tujiulize kama kila kiongozi angepangiwa muda wake na msafara wake (motorcade) hali ya msongamano ingekuwaje?

Ni muda gani ungetumika kukamilisha idadi ya viongozi wote kufika Westminster Abbey?

Hatudhani kuwa muda wa ibada ya mazishi  ungeathiriwa na misafara ya viongozi?

Ifahamike kuwa katika matukio kama lile na yafananayo na lile  utaratibu wa usafiri, malazi na usafiri huratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi husika.

Katika muktadha huu suala la usafiri wa  viongozi wa nchi na serikali liliratibiwa Ofisi ya Masuala ya Kigeni, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (Foreign, Commonwealth and Development Office/ FCDO) ya Uingereza.

Utaratibu huu hufanyika ili kurahisisha usalama wa viongozi mbalimbali duniani kwa wakati mmoja na hii ni kwa sababu itifaki na usalama wa viongozi ni mambo yanayoenda pamoja na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi kupakiwa kwenye mabasi kwa sababu hata katika  Mkutano wa Jumuiya ya Madola mwaka 2018 (CHOGM2018) uliofanyika London na Windsor viongozi kutoka nchi zaidi ya 54 walipakiwa kwenye mabasi kwenda na kurudi kwenye mikutano kwa siku zote za mikutano.

Hayo yamekuwa yakifanyika hata Tanzania pia labda kwa bahati mbaya wengi huwa hawafuatilii.

Hivyo si dhihaka kama wengi wanavyodhani bali ni sehemu ya utaratibu katika kurahisisha usalama wa viongozi.

Zaidi, kitendo hiki cha kuwapatia usafiri mmoja viongozi hutoa nafasi kwa viongozi kuyasoma mazingira ya nchi au eneo husika na wao kupata muda wa kuchanganyika na kubadilishana mawazo ambapo kitendo hicho huitwa poding.

Wenu:

Abbas Mwalimu

(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).

+255 719 258 484.

Uwanja wa Diplomasia

(Facebook|WhatsApp).

error: Content is protected !!