Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Suluhu Sports Academy Mkunguni-Kizimkazi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa michezo na wananchi. Katika hotuba yake, Rais Samia amezungumzia umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.
Vijana na Miundombinu
Rais Samia ameanza kwa kusisitiza umuhimu wa kujenga miundombinu kwa ajili ya vijana wa Tanzania. “Kama tunavyofahamu, asilimia kubwa ya watu wa Tanzania ni vijana, na vijana hawa wanahitaji kujengewa miundombinu kadhaa ya shughuli zao kiuchumi, kiafya, utamaduni lakini pia mambo yao mengine,” alisema Rais Samia, akielezea umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujenga mustakabali wao.
Tamasha la Kizimkazi na Ujenzi wa Suluhu Academy
Akiendelea, Rais Samia aligusia mafanikio ya Tamasha la Kizimkazi la mwaka 2024, akisema tamasha hilo limejibu mahitaji ya vijana, na mradi wa Suluhu Academy ni sehemu muhimu ya kuimarisha mustakabali wa vijana nchini. “Mradi huu unabeba taswira pana na ndoto kubwa ya vijana wetu wa sasa na kizazi kijacho, hususani wale wenye vipaji vya michezo,” aliongeza Rais Samia, akiweka wazi kuwa michezo sasa ni zaidi ya burudani kwani imekuwa ajira, biashara na chanzo kikubwa cha utalii.
Ajira na Wakandarasi wa Ndani
Katika hotuba yake, Rais Samia aliwashukuru wakandarasi wanaoendesha ujenzi huo kwa kuitikia wito wa kutumia wakandarasi wa ndani. “Tunawakandarasi wenye sifa za kutosha wanaoweza kufanya maendeleo yetu,” alisema, huku akibainisha kwamba ujenzi wa uwanja huo tayari umeanza kuleta ajira, na zaidi zitapatikana baada ya ujenzi kukamilika. Aliwasihi wataalamu kuanza kujitayarisha kwa ajira zitakazotokana na uendeshaji wa uwanja huo.
Uwanja wa Taifa
Rais Samia alifafanua kuwa uwanja huo sio wa kusini mwa Unguja au Zanzibar pekee, bali ni wa taifa zima. “Uwanja huu umeshirikisha wadau wengi na ni uwanja wa taifa la Tanzania,” alisema, akifurahia kuwa uwanja huo unajengwa kwa viwango vya FIFA.
Vilabu vya Michezo na Wawekezaji
Rais Samia pia alizungumzia mchango wa vilabu vya michezo na wawekezaji katika mradi huo. Alisema, “Nimeongea na wadau, mmoja nimempa Yanga, mmoja nimempa Simba awasaidie. Litakapokamilika, tutaitana vilabu tuambizane.”
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwahimiza wakandarasi na wadau wa mradi huo kutekeleza majukumu yao kwa kutambua kwamba wanabeba ndoto za vijana wenye vipaji na matumaini ya ukuaji wa fursa za utalii na biashara kubwa nchini.