Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Zimamoto na Hospitali ya Muhimbili sambamba na menejimenti ya maafa kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kuokoa watu walionaswa katika kifusi cha ghorofa lililoporomoka asubuhi ya leo, Novemba 16 Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Akiandika katika kurasa za mitandao ya kijamii za Instagram na X, Rais Samia pia ameagiza uongozi wa Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili kuhakikisha majeruhi wanapatiwa matibabu.
“Nimesikitika kupokea taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
Nimeuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi.
Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia utulivu na subra ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii.”