Wakulima kufaidika na punguzo bei ya mbolea

HomeKitaifa

Wakulima kufaidika na punguzo bei ya mbolea

Wakati Serikali ikitarajia kuanza kutoa ruzuku katika pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea, wakulima wametakia kufuata utaratibu ulioweka ikiwemo kujisajili ili kufaidika na fursa hiyo itakayopungizia gharama za uzalishaji.

Kupitia mpango huo wa ruzuku, mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122, 695 zitauzwa kwa Sh70 000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh52,695.

Pia UREA (ya kukuzia) iliyokuwa inauzwa kwa Sh124,734 wakulima wataenda kuinunua kwa Sh70,000.

Wakati akifunga Sherehe za Wakulima za Nane Nane Agosti 8 mwaka huu, Rais Samia aliagiza mpango huoa uanze Agosti 15 ili kuwawezesha wakulima kujianda vema na msimu wa kilimo unaokuja.

Wakulima wafanye nini?

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Saba Saba mkoani  Njombe Agosti 10, 2022 amesema zipo hatua kadhaa ambazo mkulima anatakiwa kufuata ili apate punguzo la bei ya mbolea.

Hatua ya kwanza, wakulima wahakikishe wamejisajili ili waweze kupata mbolea kwa bei ya punguzo iliyotolewa na Serikali.

“Mkulima ukienda dukani swali la kwanza utakaloulizwa umejisajili? Hata kama hujajisajili mwambie ukweli sijajiajili,” amesema Bashe.

Kama mkulima hujajisajili, wakala wa mauzo atakuelekeza mahali pa kujisajili ambapo atachukua taarifa za mkulima ikiwemo majina kamili,  kukupiga picha, kuchukua alama ya kidole gumba na namba ya simu.

“Ni muhimu uweke namba yako ya simu ili sisi ili tujiridhishe kama umenunua huo mfuko,” amesema Bashe.

Hatua ya pili mkulima ni lazima ahakikishe mfuko anaonunua una nembo ya ruzuku pamoja na msimbo wa majibu ya haraka (QR code) ambayo itakuwepo kwenye kila mfuko kuthibitisha kwamba huo mfuko wa mbolea umelipiwa ruzuku na Serikali.

“Utaona kidude pembeni ambacho kina na stika ukiona na mbolea haina hicho kitu toa taarifa kwa viongozi wa Serikali waliopo jirani hiyo ni mbolea ya usaniii iliyobanduliwa neno ruzuku,” ameongeza Bashe.

Amesema hatua hizo zikifuatwa vizuri zitapunguza wizi wa fedha kutoka kwa wakulima kuuziwa mbolea kwa bei ya juu ambayo tayari imelipiwa ruzuku.

Mawakala, makampuni ya mbolea waonywa

Waziri Bashe amewataka  mawakala wa mbolea kutumia mfumo mpya wa uuzaji wa mbolea kwa kutumia mashine za kielektoniki za mauzo na malipo (POS machine) ili kuwezesha ufanisi wa mfumo wa ruzuku.

“Mawakala wote ni lazima wawe na mfumo wa POS, sisi tumeshatoa msimbo wa QR kila mfuko utabandikwa neno ruzuku na huo msimbo unaotofautisha mfuko mmoja na mwingine,” amesema Waziri.

Mashine hizo zitafanya kazi ya kuskani msimbo utakaobandikwa kwenye kila mbolea wenye uwezo wa kutofautisha mfuko mmoja wa mbolea na mwingine.

Wakala atatakiwa kuingiza taarifa za mkulima kwenye mashine ya POS, na taaarifa hizo zitamuwezesha kupata ruzuku ya Serikali kwenye kila mfuko aliouza.

“Mtu akijifanya kuskani mfuko aufiche ndani  alafu  aje aurudie mara ya pili itakuwa imekula kwakwe kwa sababu namba ile ikishaskaniwa mara moja haiwezi kurudiwa mara ya pili,” ameongeza Bashe.

Aidha Waziri Bashe amewahakikishia wauzaji wa mbolea nchini kwamba malipo yao yapo tayari, hivyo wahakikishe bei ya mbolea ni moja nchi nzima.

Sambamba na hilo amemshukuru Rais Samia kwa maamuzi ya kutoa ruzuku hiyo itakayoenda kusaidia wakulima kuzalisha zaidi.

“ Ni maamuzi yanayolinda usalama wa nchi na ukuaji wa uchumi na kuwasaidia wanachi wengi wanaolima kuondokana na janga la umaskini,” amesema Bashe.

error: Content is protected !!