TCU, UTUMISHI MBADILIKE

HomeElimu

TCU, UTUMISHI MBADILIKE

Hivi karibuni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Jenista Mhagama ametangaza kuwa zaidi ya nafasi za ajira takribani 40,000 zitatotelwa kwenye taasisi na mashirika mbalimbali ya kiserikali na hivyo watu kukaa mkao wa kula.

Ajira hizo kwakweli zimeanza kuonekana. Ukigeuka huku kuna TRA, huku kuna VETA, NCAA, hujakaa sawa TSN, mara Chuo Kikuu cha Mzumbe, CBE, UDSM,  TIE n.k. Kwa ufupi nafasi za ajira zimekuwa na nyingi sana.

Hii ni hatua nzuri sana kwa Serikali ukitathmini kuwa idadi hii wa waajiriwa inaenda kupunguza kwa asilimia kubwa tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini.

Changamoto zinaibuka kwa baadhi ya watu kupata nafasi hizi za kazi. Awali ilionekana tatizo kwa wale waliosoma vyuo vikuu nje ya nchi, lakini sasa tatizo limesogea kabisa mlangoni hadi kwa wale waliosoma vyuo vya ndani ya nchi.

TATIZO NI NINI HASA?

Wapo watu ambao husoma nje ya nchi, yaweza kuwa nchi jirani na wengine nje ya Bara la Afrika kabisa na baada ya kuhitim hurudi nchini  ili waweze kutumia elimu waliyoipata nje kama waajiriwa wa sekta mbalimbali ndani ya serikali. Habari mbaya ni kwamba juhudi hizo hugonga mwamba kwani hata pale wapatapo  uthibitisho wa vyeti vyao (Veification Certificate) kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) bado watakosa nafasi za kazi kwani Utumishi huishia kuangalia lililopo kwenye cheti cha mwombaji aliyesoma nje na kama halifanani moja kwa moja na vyeti vya ndani hawajichoshi hata kufuatilia ‘trascript’ kuona je kwenye kozi ya jina hilo mhitimu amesoma nini?

Hali hii hupelekea wahitimu waliosoma nje kuishia kujiajiri ama wengi kuajiriwa na kampuni binafsi na kuelekeza ujuzi wao kwenye sekta hizi ambazo huonekana kuwa na mafanikio zaidi na hii ni kutokana na kuwa na watu wenye ujuzi tofauti tofauti kutoka sehemu mbalimbali za dunia ambao hukutana na kufundishana mbinu hizo kisha kufanya kazi kwa lengo moja.

Si, kwamba elimu inayotolewa nchini ni mbovu, la ha sha! Ni kwamba unapochanganya watu wenye ujuzi tofauti tofauti kutoka sehemu tofauti tofauti husaidia wao kugawana ujuzi na kufanya kazi ziende kwa ufanisi zaidi

Hii iko wazi ndio maana mtu aliyefanya kazi na kampuni mbalimbali ana ‘experience’ ya kutosha kuajiriwa sehemu nyingi kwani amefanya kazi na watu tofauti tofauti hivyo kumsaidia kuongezea ujuzi alionao.

Ukifuatilia watu wengi watakuambia hakikisha umejaza taarifa zako kwenye tovuti ya ajira (ajira portal) walau kwa 80%, si wengi wameweza kukamilisha vigezo vinavyohitajika kwa 100% lakini pia utagundua wapo wale waliofanikiwa na bado wapo mtaani kwasababu mbalimbali ikiwemo hiyo ya kuwa amesoma nje ya nchi.

Janga hili la watu wenye vigezo kushindwa kupata ajira lipo ndani ya nchi pia kwani moja wa wahitimu wa kozi iliyoanzishwa mwaka 2015 katika Chuo Kikuu Tumaini Makumira. Mhitimu huyo wa kozi ya  ‘Bachelor of Education in Primary Education’ ambayo wahitimu wake wa kwanza walihitimu mwaka 2018 ameelezea dukuduku lake leo kupitia Clouds FM na kuelezea namna ambavyo uombaji wa ajira umekuwa changamoto kwani kwenye mfumo wa sekretarieti ya ajira kozi hiyo haijaorodheshwa na hata ile ya ‘Early Childhood Education ambayo ipo kwa muda mrefu sasa ndio kwanza imewekwa hivi karibuni.

Nafasi za ajira huja na kisehemu ambacho huorodhesha watu ambao wanaweza kuomba nafasi hiyo ni watu wenye vyeti vya aina gani, lakini pia huongezea na related field kwa wale ambao wamesoma vitu vinavyoendana na vile vilivyoorodheshwa lakini sidhani kama hii huwekwa maanani.

Maswali yapo kwa vijana wengi ambao wanatamani kupata ajira hizi, Je! Taarifa za uanzishwaji wa kozi hizi huwafikia Utumishi kwa wakati? Kama haziwafikii, Je! TCU inazitambua kozi ambazo hazijaorodheshwa kwenye mfumo na zina wahitimu? Kwa mfano, je TCU wanafahamu kuwa kuna wahitimu kutoka Chuo Kikuu Tumaini Makumira katika kozi ya ‘Bachelor of Education in Primary Education’ ambao wamehitimu toka mwaka 2018, 2019, 2020 na 2021 ambao ambao mfumo wa Utumishi hawawatambui hivyo HAWAAJIRIKI.

Je kuna haja ya Tanzania kuwa na wahitimu wa Kitanzania kutoka nje ya nchi? Je! Nini kinafanyika ili wahitimu hawa kutoka vyuo vinavyofahamika na kukubalika na TCU wenye ujuzi wa kozi zilezile zilizopo nchini lakini kwa jina tofauti kuweza kuangaliwa na kupata ajira? Lengo la kuambatanisha nakala za vyeti na matokeo ‘transcript’ wakati wa kuomba kazi ni lipi ikiwa mfumo haujabadilishwa kukubali baadhi ya vyeti?

Ombi ni kwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora) – Jenista Mhagama na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia – Prof. Adolf Mkenda kuangalia suala hili kwa jicho la pili ili kusudi wizara hizi mbili zishirikiane kuhakikisha watu wenye elimu inayotakiwa kwa nafasi za ajira zinazotolewa wanapata nafasi ya kufanya maombi hayo huku wakitilia maanani kozi mpya zinazoanzishwa vyuoni lakini pia wananchi wanaosoma nje kwa lengo la kupata ujuzi walionao wenzetu na kuuleta nchini kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

error: Content is protected !!