KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Chama cha Mapinduzi, kimedhamiria kuwa uchaguzi ujao utakuwa ni wa uadilifu na kwamba wanataka chama kisafi ambacho kitakuwa tayari kuwatumikia wananchi.
Dk. Nchimbi amesema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma yenye kaulimbiu yake isemayo ‘Shiriki uchaguzi kwa uadilifu, na kazi iendelee’
“Mkutano mkuu umesisitiza kwamba tunataka uchaguzi wa uadilifu, na kwakweli tungependa wana-CCM wote watuelewe tukisema uadilifu, mwenyekiti anamaanisha, kamati kuu inamaanisha na halmashauri kuu inamaanisha. Tunataka chama kisafi ambacho kiko tayari kutumikia wananchi”
Aidha, Dk John Nchimbi amesema sherehe hii imefanyika mwaka huu badala ya mwaka 2027, kufuatia maombi kutoka mikoa mbalimbali iliyotambua mafanikio makubwa ya Serikali chini ya chama hicho.