Bandari ya Bagamoyo haijauzwa

HomeKitaifa

Bandari ya Bagamoyo haijauzwa

Serikali ya Tanzania imekanusha uvumi unaodai kuwa mamlaka zake zimeuza Bandari ya Bagamoyo kwa Kampuni ya Uwekezaji na Maendeleo ya Saudi Arabia (SADC).

Uvumi huo ulienea baada ya kusambaa kwa picha katika mitandao ya kijamii zikimuonesha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, akiwa pamoja na ujumbe wa wawekezaji kutoka Saudi Arabia na viongozi wa serikali. Baadhi ya taarifa zilidai kuwa picha hizo zilikuwa sehemu ya makabidhiano rasmi ya bandari hiyo.

Aidha, Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA) lilimnukuu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Saudi Arabia, Hassan Al-Huwaizi, akidai kuwa Tanzania imeipa SADC haki za umiliki na uendeshaji wa Bandari ya Bagamoyo.

Hata hivyo, afisa mwandamizi wa serikali, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amekanusha madai hayo akisema:

“Taarifa hiyo haina ukweli. Ni kweli kwamba viongozi wa Bandari ya Tanzania na baadhi ya Mawaziri walihudhuria mkutano na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, lakini kilichojadiliwa ni mpango wa kibiashara wa pamoja, si uhamishaji wa umiliki wa bandari.”

Afisa huyo alifafanua kuwa makubaliano yaliyofanyika yalikuwa ya ishara tu, na hakuna mkataba wowote rasmi uliosainiwa kuhusu umiliki wa bandari hiyo.

“Tunapenda kuufahamisha umma kuwa picha zilizosambaa zilihusiana na majadiliano ya uwekezaji, si makabidhiano rasmi. Kutakuwa na hafla rasmi ya utiaji saini endapo pande zote mbili zitakubaliana kwa mujibu wa taratibu za kisheria,” aliongeza.

Mpango wa uwekezaji wa Saudi Arabia katika Bandari ya Bagamoyo ni sehemu ya mradi wa East Gateway Project, unaolenga kuimarisha nafasi ya Saudi Arabia kama kitovu cha biashara duniani na kuongeza uwekezaji wake barani Afrika.

error: Content is protected !!