Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia azimio la Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuwasimamisha kudhuria mikutano miwili wabunge Askofu Gwajima na Jerry Silaa baada ya kuwatia hatiani.
Wabunge hao waliitwa mbele ya kamati hiyo wiki iliyopita kujibu kuhusu matamshi waliyoyatoa wakiwa nje ya Bunge.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka amenukuliwa mbele ya Bunge akisema kuwa Gwajima na Silaa ni wajeuri, wakaidi lakini pia ni watu ambao wameonesha kutojutia hata kidogo kauli walizotoa.
Wabunge kadhaa waliochangia wamependekeza kuwa licha ya adhabu hizo kuna haja bado ya kufuatilia kwa karibu mienendo ya wabunge hao nje ya Bunge huku baadhi wakipendekeza Askofu Gwajima achunguzwe na vyombo vingine kwa makosa ya uchochezi na upotoshaji.
Kamati pia imependekeza Gwajima afikishwe mbele ya kamati ya CCM kwa mahojiano kuhusu mwenendo wake na Jerry Silaa asimamishwe mikutano pamoja kusimamishwa uwakilishi wa Bunge la Afrika (PAP).