Mgonjwa aliyedumu na tezi dume kwa miaka miwili afanyiwa upasuaji na Kambi ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia

HomeKitaifa

Mgonjwa aliyedumu na tezi dume kwa miaka miwili afanyiwa upasuaji na Kambi ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia

Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia imefanikiwa kutatua changamoto ya ugonjwa wa tezi dume kwa Bw. Athuman Rashid (78), mkazi wa wilaya ya Pangani kijiji cha Magodi ambaye ameishi na ugonjwa huo kwa miaka miwili akipata haja ndogo kwa njia ya mpira.

Upasuaji huo umefanyika Mei 16, 2025 Mkoani Tanga, Wilaya ya Pangani uliongozwa na Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Dkt. Tito Lyimo akisaidiana na madaktari na wataalam wengine kutoka hospitali ya wilaya ya Pangani.

Dkt. Lyimo amesema Bw. Athumani alikuwa akibadilisha mpira wa haja ndogo kila baada ya wiki mbili kwa miaka miwili tangu alipogundulika ana ugonjwa wa tezi dume.

Kwa upande wake Bw. Athumani amesema ugonjwa ulianza kujitokeza kwa dalili za kukojoa mara kwa mara usiku na baada ya miezi miwili mkojo uliziba na ndipo alipokimbizwa hospitali na kuwekewa mpira na kupewa maelekezo ya kubadili mpira kila baada ya wiki mbili.

“Tulitafuta matibabu katika hospitali tofauti tofauti na nilishindwa kupata matibabu ya kudumu kutokana na hali duni hivyo kushindwa kumudu gharama kubwa za upasuaji,” amesema Bw. Athumani.

Aidha, Bw. Athumani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka madaktari bingwa wilaya ya Pangani na kuongeza kuwa madaktari hao wamekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania ambao asilimia kubwa wamekuwa wanashindwa kupata matibabu kutokana na umasikini na umbali wa kufuata huduma.

error: Content is protected !!