Laini za simu 47,728 zafungiwa kwa uhalifu, ulaghai mtandaoni

HomeKitaifa

Laini za simu 47,728 zafungiwa kwa uhalifu, ulaghai mtandaoni

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebaini kuzifungia laini za simu 47,728 na Nambari za Kitambulisho cha Taifa (NIDA) 39,028 zilizohusika katika kufanya uhalifu na ulaghai mtandaoni.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kudhibiti matumizi haramu ya huduma za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa mtandaoni na ulaghai wa kupitia mitandaoni ya kijamii.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Alisema kwa kutumia mfumo wa kusimamia mawasiliano TCRA imefanikiwa kubaini shughuli hizo haramu na kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, operesheni za ukaguzi zilifanikisha kukamatwa kwa vifaa 42 vilivyokuwa vikitumika kufanya uhalifu wa uchepushaji wa simu za kimataifa. Operesheni hii ni endelevu na inakusaidia kulinda mapato ya serikali na usalama wa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini,” alisema.

Silaa alisema katika juhudi nyingine za kudhibiti uhalifu wa mitandaoni, TCRA imeendelea kusimamia kanzidata namba yambulishi ili kubaini na kufungia vifaa vya mawasiliano vilivyonakiliwa, kutumika kwa udanganyifu au vilivyoripotiwa kupotea au kuibiwa.

Alisema jumla ya namba tambulishi 44,306 zilifungiwa katika kipindi hicho.

error: Content is protected !!