Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa miradi yote ya maji imelenga kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, lakini pia ni muhimu kulinda mazingira ya Ziwa Victoria ambalo ni muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya kibiashara katika Jiji la Mwanza na maeneo jirani.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo mara baada ya kuzindua rasmi Mradi wa Chanzo cha Maji Butimba, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 71.6, akisema kuwa mradi huo utaboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani.
“Maziwa Makuu ikiwemo Ziwa Victoria ni vyanzo vya uhakika vya maji kwa matumizi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, hivyo niwakumbushe kuwa suala la uhifadhi wa mazingira ikiwemo kudhibiti kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Victoria ni msingi wa uendelevu wa upatikanaji wa maji, kuwezesha shughuli mbalimbali za maendeleo kama vile kilimo, viwanda, ufugaji, uvuvi, utalii na usafiri kwa njia ya maji,” Rais Samia amesema.
“Kwa muktadha huo, Naagiza juhudi za kuhifadhi mazingira ziendelee kufanyika kikamilifu kwa kushirikisha sekta zote,” Rais Samia ameagiza
Aidha, Rais Dkt. Samia amefurahishwa na mradi kuhusisha ujenzi wa vyoo vya kisasa vya umma vipatavyo 107 katika mashule, zahanati na masoko katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela. Akisema kuwa ni dhahiri kuwa programu hii ya LVWATSAN imegusa maisha ya kila siku ya wananchi wa Jiji la Mwanza.
Pia, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Mradi huu umetekelezwa kupitia Programu ya Lake Victoria Water and Sanitation (LVWATSAN) kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Française de Développement – AFD). Akitoa shukrani kwa Washirika na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano wao na Serikali katika kuleta maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kupitia programu ya LVWATSAN awamu ya kwanza, miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya namna hii imetekelezwa na kukamilika katika Miji ya Magu na Misungwi Mkoani Mwanza, pamoja na Mji wa Lamadi.