Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian amesema mkoa huo unahifadhi ya lita za ujazo milioni 210 za mafuta ya petroli na dizeli, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya nishati.
Akizungumza mkoani Dodoma Julai 15, 2025 Dk. Burian amesema mafuta hayo yanahifadhiwa kwenye matenki ya Kampuni ya GBP, yakitumika kusambaza nishati kwa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, hatua inayopunguza gharama za usafirishaji na kupunguza bei kwa watumiaji.
Amesema maendeleo hayo ni sehemu ya fursa mpya za kiuchumi zinazochochewa na Serikali ya Awamu ya Sita, huku Tanga pia ikisonga mbele kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo taasisi za Serikali 1,493 zenye watumiaji zaidi ya 735,000 zimetambuliwa.
Kuhusu mradi wa bomba la mafuta ghafi (EACOP), Balozi Batilda amesema ujenzi wa miundombinu unaendelea vizuri na umefikia asilimia 53, huku wananchi 1,560 kati ya 1,580 waliopisha mradi huo wakinufaika kwa kulipwa fidia ya zaidi ya Shilingi Bilioni 9.3.