Ofisi ya Msajili ya Vyama vya Siasa imesema wagombea urais wamewekewa ukomo wa kutumia Sh bilioni tisa kugharamia uchaguzi.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Ofisi hiyo, Muhidin Mapejo alisema wakati wa mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa.
“Kama unataka kwenda kufanya kampeni zako ukomo wako wa matumizi usivuke bilioni tisa (shilingi). Kama wewe utakuwa na milioni 100 maana yake ni kwamba hata utakapokuwa unakwenda kwenye kampeni zingine, ukimpata mtu akachanga isivuke bilioni tisa,” alisema Mapejo.
Kwa upande wa wagombea wa ubunge, ukomo kwenye majimbo umezingatia idadi ya watu, ukubwa wa majimbo, miundombinu ya majimbo hivyo kuna viwango tofauti na kiwango cha juu ni shilingi milioni 136.
Mapejo alisema wagombea udiwani wamewekewa ukomo wa kutumia sh milioni 16 kwenye kampeni zao.
“Kama utaona kwamba mimi siwezi kufika milioni 16 labda nitakuwa na milioni tatu, milioni nne ama milioni tano hizo unaruhusiwa kutumia, cha msingi ulijaza fomu na fomu yako ilisema kwamba ni milioni 16,” alisema Mapejo.
Aidha, utaratibu huo utasaidia kudhibiti vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika kipindi cha uchaguzi.