Mkurugenzi wa MashtakaTanzania (DPP), amewafutia kesi na kuwaachia huru washtakiwa 210 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda kosa la uhaini.
Washtakiwa hao wameachiwa leo Novemba 24, 2025 katika Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza walilokuwa wamefikishwa kwa nyakati tofauti katika Mahakama hizo.
Itakumbukwa Novemba 14,2025 akizindua Bunge la 13, jijini Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan alimwagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasamehe vijana waliofanya makosa kwa kufuata mkumbo.
“Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamilia kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,” alisema Dkt Samia.
Jijini Mwanza leo jumla ya watuhumiwa 139 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini,ikiwemo kuchoma moto, kuharibu mali za umma, na unyang’anyi wa kutumia silaha kutokana na vurugu pamoja na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 waliachiwa huru baada ya DPP kuondoa kesi zao mahakamani.
Katika orodha hiyo, 76 walifutiwa mashtaka kutenda kosa (uhaini), wilayani Ilemela, wakati 63 walitoka Nyagamana wakishtakiwa kwa kuharibu mali kwa makusudi, unyang’anyi wa kutumia silaha na kuchoma moto.
Wote wamefutiwa mashtaka hayo leo Jumatatu Novemba 24, 2025 katika Mahakama za Wilaya ya Ilemela na ile ya Nyamagana.
Uamuzi huo umekuja baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya DPP wa kuonesha nia ya kutoendelea kuwashtaki na mashtaka hayo.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam DPP amewafutia kesi na kuwaachia huru washtakiwa 47 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutenda na kosa la uhaini.
Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema akishirikiana na Cathbert Mbiling’i waliileleza mahakama hiyo, leo Jumatatu.
Mrema alitoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, katika mahakama hiyo, kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo kwa washtakiwa 47 kati ya washtakiwa 48 waliopo katika kesi hiyo.
Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,pia imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini washtakiwa 24 waliokuwa wakishtakiwa kwa makosa mawili ya kula njama ya kutenda kosa na uhaini.
Uamuzi huo umefikiwa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erasto Philly, baada ya Mawakili wa Serikalii kuieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea kuwashitaki washtakiwa hao.


