Klabu ya Yanga imetangaza kuachana na aliyekuwa afisa mhamasishaji wao, Juma Khatib Nugaz, maarufu kama Antonio Nugaz i.Uongozi wa Yanga unasema umeamua kutoongeza mkataba na mzaliwa huyo wa jiji la Tanga aliyewahi kuvuma kwa jina la ‘Swahiba Mtembezi’.
Japo taarifa rasmi ya Yanga inasema kwamba sababu ya kuachana na Nugaz ni kumalizika kwa mkataba, kulikuwa na viashiria vya Yanga kuachana na Nugaz, siku chache baada ya Yanga kumwajiri Haji Sunday Manara katika kitengo cha Habari na Mawasiliano.
Iko hivi :
Antonio Nugaz aliajiriwa na Yanga miaka miwili iliyopita kama afisa mhamasishaji, wakati mwingine pia akijitambulisha kama msemaji wa ‘Timu ya Wananchi’.Aliacha kazi ya utangazaji (Clouds Media Group) na kutangaza kwamba Yanga wanampa heshima kubwa. Katika kutekeleza majukumu yake, Nugaz alionekana kama mpinzani mkubwa wa Haji Manara ambaye wakati huo alikuwa Simba. Mara nyingi, wamesikika wakitupiana ‘madongo’ mchana kweupe.
Mara Yanga wakamwajiri ‘Bugati’ Manara, aende kufanya kazi na Swahiba Nugaz (“Waape Salaam”). Maswali yakaanza kuibuka, watu wakihoji, mafahari hawa watakaa zizi moja? Je! watapikika chungu kimoja?.
Hazikupita siku nyingi Antonio Nugaz, akanonekana akihamasisha mashabiki wa Yanga kuwazodoa Simba. Akasema “Na ‘msukule’ wao…. tumemchukua”. Jina ‘msukule’ likaleta tabu, pale ambapo ilionekana anaamanisha ‘Bugati’ Haji Manara ndiye ‘msukule’.
Kupitia kipindi cha Joto Kali la Asubuhi kilichorushwa na kituo cha EFM Agosti 30, 2021, mtangazaji Maulid Kitenge alisema viongozi wa Yanga wamechukizawa mno na kitendo cha Nugaz.Kitenge ambaye alikuwa msherehesaji kwenye tamasha la Yanga (Siku ya Mwananchi) alisema hiyo ndiyo sababu iliyofanya Antonio asionekane kwenye tamasha hilo, na hakuwepo kabisa kwenye ratiba.
Siku chache baadae, Yanga wametangaza kuachana na Nugaz na kubakisha swali; Je! Manara ndiye sababu ya Yanga kuachana na Nugaz?.
Click Habari iko hapa kukuhabarisha kila kitakachojiri