Serikali ya Tanzania imekosoa ripoti za Amnesty International (AI) na Human Rights Watch (HRW) kuhusu matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ikizitaja kuwa za upande mmoja na zenye upendeleo wa kisiasa.
Ukosoaji huo uliwasilishwa Machi 12 katika kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), kufuatia kauli za mashirika hayo kukiri kuwa ripoti zao hazikujumuisha kikamilifu mitazamo ya serikali.
Serikali ilisema madai ya matumizi makubwa ya nguvu katika kudhibiti vurugu za uchaguzi hayakuzingatia mazingira halisi ya matukio, ikisisitiza kuwa vyombo vya usalama vilichukua hatua za kisheria kulinda maisha ya watu, mali na utawala wa sheria.
Katika mjadala huo, baadhi ya washiriki wakiwemo wawakilishi kutoka Zimbabwe walihoji uadilifu na weledi wa mashirika hayo katika kuandaa ripoti zao.
Serikali pia ilieleza kuwa wakati wa uchaguzi mitandao ya kijamii ilijaa taarifa za uchochezi na kauli za kuchochea vurugu kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, watu binafsi na taasisi, na kuhoji kwa nini matukio hayo hayakuonekana katika ripoti za mashirika hayo.


