Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Serikali ya Tanzania zimekubaliana katika ngazi ya wataalamu ukamilishaji wa tathmini za mwisho za mpango wa ufadhili wa Dola za Marekani milioni 375.5 (Sh. bilioni 974) baada ya kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo.
Fedha hizo zitaifanya Tanzania iwe imenufaika na mkopo nafuu wa Dola za Marekani bilioni 1.052 za kusaidia miradi ya kiuchumi na kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 563.8 za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi tangu utekelezaji wa programu hizo uanze.
Kiongozi wa timu ya wataalamu ya IMF iliyofanya ziara nchini, Nicolas Blancher alisema hayo baada ya kikao cha kuhitimisha ziara hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dar es Salaam.
Aidha, IMF imepongeza namna serikali ya Tanzania iliyoweza kukabili athari za changamoto za kiuchumi duniani ikiwemo vita ya Mashariki ya Kati kupitia sera za kifedha.


