Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, wameshuhudia utiaji saini wa mikataba minne ya ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano waTanzania na Jamhuri ya Namibia, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria na kufungua fursa mpya za maendeleo.
Mikataba hiyo ilisainiwa Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ya pande mbili yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Mikataba iliyosainiwa inahusu ushirikiano katika masuala ya ulinzi, ushirikiano kati ya Manispaa ya Zanzibar na Jiji la Swakopmund la Namibia, ushirikiano katika maeneo ya biashara pamoja na ushirikiano katika maendeleo ya biashara ndogo na za kati (SMEs).
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Rais Samia alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo kunaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania na Namibia ya kuendeleza uhusiano wao wa muda mrefu kwa kuuwezesha kuwa na matokeo makubwa zaidi ya kiuchumi na kijamii.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza biashara, uwekezaji, ubadilishanaji wa uzoefu na kuimarisha ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah alisema mikataba hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Namibia, uliyojengwa juu ya misingi ya mshikamano, urafiki na historia ya pamoja ya harakati za ukombozi wa Afrika na kusisitiza kuwa utekelezaji wake utafungua fursa mpya za ukuaji wa uchumi, maendeleo ya sekta binafsi na ushirikiano wa taasisi za umma.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo ni juhudi za Tanzania na Namibia za kubadilisha urafiki wao wa kihistoria kuwa ushirikiano wenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi. Pia ni ishara ya dhamira ya viongozi hao kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kukuza maendeleo endelevu, ajira, biashara na ustawi wa watu wao.


