Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema Tanzania na Namibia zinapaswa kugeuza uhusiano wao wa kihistoria wa kidiplomasia na mshikamano wa muda mrefu kuwa fursa za kiuchumi zitakazowanufaisha wananchi wa mataifa hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kizazi cha sasa kina wajibu wa kujenga juu ya misingi iliyowekwa na viongozi waasisi wa nchi hizo mbili.
Rais Nandi-Ndaitwah alisema Namibia itaendelea kuthamini mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi yake na alikumbushia kipindi alichoishi Tanzania na kushuhudia kwa karibu urafiki wa kipekee kati ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, na Baba wa Taifa la Namibia, Dkt. Sam Nujoma.
Alisisitiza kuwa urafiki huo wa kihistoria unapaswa kutafsiriwa kuwa maendeleo ya kiuchumi, biashara na ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kuhusu ushirikiano wa kiuchumi, Rais Nandi-Ndaitwah alisema viongozi hao walikubaliana kuwa kuna haja ya kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara na uwekezaji ili kuruhusu bidhaa, huduma na mitaji kusafiri kwa urahisi zaidi kati ya Tanzania na Namibia. Aliongeza kuwa sekta za kilimo, usalama wa chakula, mifugo na uvuvi zina fursa kubwa ambazo zinapaswa kutumiwa kikamilifu kwa kuanzisha ushirikiano wa kibiashara wenye manufaa kwa pande zote.
Aidha, alisema Tume za Pamoja za Ushirikiano pamoja na mawaziri wenye dhamana wanapaswa kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi. Alisisitiza kuwa sekta binafsi ina jukumu muhimu katika kufanikisha malengo hayo na kwamba wafanyabiashara wa Namibia wako tayari kushirikiana na wenzao wa Tanzania katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa nchi hizo mbili.


