Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) umepata ufadhili wa Shilingi bilioni 56.6 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kupanua Depo ya Gongo la Mboto, hatua inayotarajiwa kuimarisha uendeshaji wa mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) huku mtandao wake ukiendelea kupanuka jijini Dar es Salaam.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kujazia mabasi gesi asilia iliyobanwa (CNG), eneo la kuosha mabasi, maegesho, karakana, kituo cha mabasi ya BRT katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) pamoja na kituo cha mabasi ya mlisho (feeder station) katika eneo la Banana.
Utekelezaji wa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka 2027.
Baada ya kukamilika na kuanza kutumika, njia ya BRT ya Awamu ya Tatu inatarajiwa kupunguza msongamano wa magari, kuboresha muunganiko wa maeneo mbalimbali ya jiji, na kutoa huduma za usafiri wa umma zilizo za haraka, salama na zenye kutegemewa zaidi kwa wakazi wa Dar es Salaam.


