Rais Samia: Kalamu ya mwanasheria iwe nyenzo ya kulinda maslahi ya Taifa

HomeKitaifa

Rais Samia: Kalamu ya mwanasheria iwe nyenzo ya kulinda maslahi ya Taifa

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ni nyenzo muhimu katika kulinda maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa ikitumika kwa weledi na uadilifu inaweza kuzuia hasara kwa Serikali kabla hazijatokea na kusaidia kufanyika kwa maamuzi sahihi yenye manufaa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) leo Julai 13, 2026, Rais Samia amesema tofauti na kalamu yake inayohusika katika hatua za mwisho za utekelezaji wa sheria, kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ina nafasi kubwa ya kuzuia matatizo kabla hayajatokea.

Rais Samia amesema Mawakili wa Serikali wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kutoa ushauri wa kisheria kwa usahihi, uzalendo na uaminifu, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa badala ya maslahi binafsi.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha Mawakili wa Serikali kwa kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kuboresha mazingira ya kazi ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wakati huo huo, Rais Samia amemwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera kutatua changamoto zilizowasilishwa na Chama cha Mawakili wa Serikali, amesema baadhi zimeanza kupatiwa ufumbuzi, ikiwemo upatikanaji wa ofisi na viwanja jijini Dodoma na Arusha.

error: Content is protected !!