Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura ameeleza kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa, Hamza Mohammed aliyeuawa katika majibizano ya risasi na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga.
Akizungumza hii leo jijini Mwanza na waandishi wa habari, DCI Wambura amesema uchunguzi huo ulijikita katika mambo makuu matatu ambayo ni kutaka kumtambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma kwenda kufanya tukio lile na mwisho kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.
Wambura ameongeza kusema kuwa Hamza kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao ambayo inaonyesha matendo ya Al-Shabaab na makundi ya kigaidi kama “ISIS”.
Kulingana na hayo DCI Wambura amesema kwamba kitendo alichokifanya Hamza Mohammed kilikuwa ni cha ugaidi wa kujitoa mhanga.