Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema imezima mtambo wa Ruvu Juu ulioko Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kupelekea kukosa huduma ya maji kwa takribani saa 12 katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam na Pwani, leo ili kujiandaa kukabiliana na athari za mvua zinazoweza kutarajiwa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro amesema matengenezo yameanza kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, yakilenga kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa.
Kwa mujibu wa DAWASA, maeneo yanayoathirika kutokana na matengenezo hayo ni pamoja na Ruvu Darajani, Ruvu JKT, Vigwaza, Mlandizi, Mbwawa, Soga, Mwendapole, Tanita, Kwa Mathias, Picha ya Ndege, Kibaha, Kiluvya, Kibamba, Malamba Mawili, Saranga, Mbezi, Ubungo, Kimara, Tabata, Segerea, Kinyerezi, Kisukuru, Bonyokwa, Ukonga, Uwanja wa Ndege, Kiwalani, Vingunguti, Gongo la Mboto, Pugu na Kisarawe.


